43 wauawa katika makabiliano baina ya askari na wanamgambo DRC
Kwa akali watu 43 wameuawa katika siku tatu za makabiliano baina ya wanajeshi na magenge ya wabeba silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hayo yalisemwa jana Jumatatu na Gilbert Tsale, afisa wa ngazi za juu wa serikali katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa DRC ambaye alibainisha kuwa, "shambulizi baya zaidi ni la Ijumaa ambapo watu waliokuwa wamejizatiti kwa bunduki na visu waliua raia 21 katika mji wa Mahagi."
Naye Kanali James Ngongo, msemaji wa jeshi katika mkoa wa Ituri amesema makabiliano baina ya wanajeshi na wanamgambo katika eneo la Lisey tokea siku ya Jumapili yameua raia 2, askari 2 na wapiganaji 12 waliokuwa wamejizatiti kwa silaha.
John Kambale, afisa wa serikali katika eneo la Malambo karibu na mji wa Beni mkoani Kivu Kaskazini amesema genge la kigaidi la ADF liliua raia sita akiwemo mwanamke mmoj siku ya Jumapili
Haya yanajiri siku chache baada ya watu wasiopungua 17 kuuawa na wengine kadhaa kijeruhiwa katika shambulizi lililolenga gari lililokuwa na walinzi wa mbuga ya taifa na abiria kadhaa huko mashariki mwa nchi hiyo.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.