May 07, 2020 07:58 UTC
  • Mapigano ya kikabila Darfur, Sudan yaua watu 30

Kwa akali watu 30 wameuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika mapigano ya kikabila baina ya Waarabu na wasiokuwa Waarabu katika mkoa wa Darfur Magharibi nchini Sudan.

Waziri Mkuu, Abdalla Hamdok amesema mapigano hayo ya kikabila yalianza Jumanne na yakaendelea kushuhudiwa hadi jana Jumatano. Naye Hashim Mahmoud, Gavana wa mkoa wa Darfur Magharibi amesema mamlaka husika katika eneo hilo imetangaza agizo la kutotoka nje sanjari na kutuma askari zaidi katika eneo hilo kwa lengo la kujaribu kudhibiti hali.

Adam Regal, msemaji wa shirika moja la kuwasaidia wakimbizi katika eneo hilo amesema mapigano hayo yaliripuka baada ya kundi la watu wa kabila la Falata kuwaibia watu wa kabila la Kiarabu la Rizeigat, katika mji wa Rumali.

Mapema mwaka huu, watu 36 waliuawa katika mapigano mengine ya kikabila aina ya Waarabu na wasiokuwa Waarabu katika mkoa huo wa Darfur Magharibi nchini Sudan.

Mauaji na mapigano yanashuhudiwa Darfur licha ya uwepo wa askari wa kulinda amani wa UN

Umwagaji damu unaendelea kushuhudiwa katika eneo la Darfur, licha ya serikali mpya ya Sudan kuahidi kumaliza migogoro nchini humo ukiwemo ule wa Darfur ambao umepelekea watu wasiopungua laki tatu kuuawa na wengine milioni mbili na nusu kuwa wakimbizi.

Darfur ilikumbwa na mgogoro kuanzia mwaka 2003 uliohusisha kundi la waasi lililodai kutengwa na utawala wa Rais Omar al-Bashir aliyeng'atuliwa madarakani.

 

Tags