Makabila ya kaskazini mwa Misri yajiandaa kutekeleza operesheni dhidi ya ISIS
Duru za kieneo zimeripoti kwamba makabila ya eneo la Sinai, kaskazini mwa Misri yametangaza utayarifu wao wa kutekeleza operesheni dhidi ya magaidi wa kundi la Daesh baada ya kumalizika mwezi wa Ramadhani.
Mtandao wa habari wa Al-Arabi Al-Jadid umeripoti kwamba sambamba na kuongezeka mashambulizi ya magaidi wa Daesh katika kambi na mashamba yanayomilikiwa na makabila ya eneo la Sinai, makabila hayo yamekubaliana kushirikiana na jeshi la Misri katika mashambulizi dhidi ya magaidi hao wakufurishaji wa Daesh.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, magaidi wanaojiita 'Wilayat Sainaa' ambao walitangaza utiifu wao kwa kundi la Daesh (ISIS) wamekuwa wakishambulia mtu au kundi lolote lenye ushirikiano na maafisa usalama wa Misri kiasi kwamba katika mashambulizi ya hivi karibuni idadi kadhaa ya raia waliuawa na wengine kujeruhiwa.
Aidha nyumba, magari na mashamba yameteketezwa moto na magaidi hao. Mmoja wa viongozi wa makabila ya eneo la Sinai na ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema kuwa kikao cha pamoja kati ya viongozi wa makabila na makamanda wa jeshi tayari kimefanyika ambapo pia kumetolewa wazo la kuunganishwa watu wa makabila hayo katika makundi ya maafisa usalama wa serikali.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kikabila, hadi sasa watu 1000 wamejitolea kupambana na wanachama wa Daesh. Aidha jeshi la Misri tayari limekabidhi silaha kwa watu wa makabila hayo kwa ajili ya operesheni hizo.