Wanamgambo wa ADF washambulia Ituri DRC na kuua 17
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61240-wanamgambo_wa_adf_washambulia_ituri_drc_na_kuua_17
Kwa akali watu 17 wameuawa katika shambulizi la kundi la wanamgambo wa ADF huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
May 27, 2020 03:29 UTC
  • Wanamgambo wa ADF washambulia Ituri DRC na kuua 17

Kwa akali watu 17 wameuawa katika shambulizi la kundi la wanamgambo wa ADF huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Gili Gotabo, kiongozi wa asasi moja ya kiraia katika eneo la Irumu amesema idadi kubwa ya watu waliuawa katika shambulizi hilo la JUmatatu la wapiganaji wa ADF katika kijiji cha Makutano mkoani Ituru, yapata kilomita 100 kusini magharibi mwa jiji la Bunia.

Ingawaje kituo cha utafiti cha Kivu Security Tracker (KST) kimesema ni watu 17 tu waliouawa katika shambulizi hilo la kigaidi, lakini mashuhuda na viongozi wa eneo hilo wanasema waliouawa ni wengi kuliko idadi iliyotajwa.

Mwezi uliopita wa Mei, watu wasiopungua 27 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulio mawili tofauti katika mkoa wa Ituri na Kivu Kaskazini huko DRC. Shambulizi hilo lilijiri wiki chache baada ya watu zaidi ya 150 kuuawa katika mkoa wa Ituri katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika kipindi cha siku 40 zilizopita.

Mkoa wa Ituri ni katika maeneo ya DRC yanayoshuhudia hujuma za kila mara za waasi na magaidi

Mamia ya Wakongomani wameuawa katika mashambulizi ya wanamgambo wa ADF ambao asili yao ni Uganda hususan katika maeneo ya mashariki mwa nchi, tokeo mwaka 2014. 

Eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi.