Uzinduzi wa miradi ya ustawi wa uchumi wa kidijitali nchini Iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo ameshiriki katika uzinduzi wa miradi minne ya miundo msingi wa kidijitali ya Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Miradi hiyo ambayo imezinduliwa katika mikoa ya Azarbaijan Mashariki, Tehran, Khorassan Razavi na Fars inalenga kuimarisha mfumo wa kitaifa wa kidijitali ili nchi hii iweze kujitegemea na kukabiliana na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani. Miongoni mwa miradi iliyozinduliwa ni ule unaohusu kuunga mkono biashara za kidijitali ambazo zimeathiriwa na janga la COVID-19 na pia mradi wa televisheni ya intaneti kwa lengo la ustawi wa kiuchumi katika uga wa kuhimiza utengenezaji bidhaa za utamaduni wa Kiirani.
Akizungumza katika uzinduzi huo ambao ulifanyika kwa njia ya video, Rais Rouhani amesema mtandao wa intaneti ni muhimu katika kutoa huduma kwa wananchi katika sekta mbali mbali kama vile kilimo na afya na kuongeza kuwa: "Katika uga wa uchumi wa kidijitali, utumizi wa intaneti katika kutoa huduma hurahisisha mambo na kupelekea kazi ifanyike kwa haraka, ubora na gharama ya chini.
Rais Rouhani ameongeza kuwa, kipindi hiki kigumu cha kuenea ugonjwa wa COVID-19 ni fursa nzuri kwa wananchi kutumia zaidi teknolojia ya inteneti kufanya kazi mbali mbali.