Morocco yapinga pendekezo la Misri kuhusu Libya
Serikali ya Morocco imepinga mpango wa Misri kuhusu Libya na kusisitiza kuwa muafaka wa kisiasa wa al Sakhirat ni marejeo asili ya ufumbuzi wa mgogoro wa Libya.
Nasser Burita Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco amesema katika mazungumzo yake ya simu na Muhammad al Taher Siyala Waziri wa serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya kwamba mapatano ya kisiasa yaliyosainiwa katika mji wa al Sakhirat Morocco ni marejeo asili ya kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa Libya na kusisitiza juu ya udharura wa kufanyika uratibu na mashauriano endelevu kati ya nchi mbili hizo katika uwanja huo.
Masuala mengine yaliyoshauriwa katika mazungumzo hayo ya simu ni pamoja na kuchunguzwa matukio ya karibuni ya kimaidani na kisiasa baada ya kukombolewa mji wa Tarhouna kutoka mikononi mwa wanamgambo wanaoongozwa na Haftar.
Rais Abdel Fattah al Sisi alitangaza baada ya kikao cha Jumamosi wiki hii huko Cairo na Khalifa Haftar kamanda wa askari wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya na Aguila Saleh Spika wa bunge lenye makao yake mashariki mwa Libya kwamba wameafikiana kuhusu mpango wa kusimamisha vita huko Libya.
Misri ni moja ya nchi zinazoliunga mkono bunge lenye makao yake huko Tobruk na wanamgambo wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar. Serikali ya muafaka wa kitaifa ya Libya siku kadhaa zilizopita ilifanikiwa kuwarudisha nyuma wanamgambo wa Haftar huko Tripoli. Aidha hapo jana serikali ya muafaka wa kitaifa ya Libya ilipinga pendekezo hilo lililotolewa na Misri na Jenerali Khalifa Haftar.