Afrika Kusini yafungua shule licha ya hofu ya wazazi na walimu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61485-afrika_kusini_yafungua_shule_licha_ya_hofu_ya_wazazi_na_walimu
Wanafunzi nchini Afrika Kusini wameanza kurejea shuleni Jumatatu ya leo baada ya skuli hizo kufungwa kwa miezi kadhaa kutokana na janga la corona.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 08, 2020 12:18 UTC
  • Afrika Kusini yafungua shule licha ya hofu ya wazazi na walimu

Wanafunzi nchini Afrika Kusini wameanza kurejea shuleni Jumatatu ya leo baada ya skuli hizo kufungwa kwa miezi kadhaa kutokana na janga la corona.

Shule hizo zimefunguliwa licha ya miungano ya walimu na wazazi nchini humo kueleza wasi wasi wao wa kuchukuliwa hatua hiyo, wakisisitiza kuwa hatua madhubuti hazijachukuliwa za kuwahakikishia wanafunzi hao usalama wao wakiwa madarasani.

Waziri wa Elimu ya Msingi nchini humo Angie Motshekga amesema, nchi hiyo itaendelea na mpango wake wa kufungua tena shule kwa ajili ya wanafunzi wa ngazi maalum baada ya kusitisha masomo kwa zaidi ya miezi miwili. Amesema asilimia 95 ya shule zimepewa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Awali, Idara ya Elimu ilipanga kufungua tena shule tarehe Mosi mwezi huu, lakini iliakhirisha mpango huo mpaka hii leo Juni 8 baada ya kugundua kuwa shule nyingi zilihitaji muda zaidi kufanya maandalizi ya kuanza tena masomo ili kutimiza hatua za afya, usalama, na kuweka umbali kati ya wanafunzi.

Kesi za corona zimekithiri katika nchi za Afrika

Waziri Motshekga amesema, wamefanya na wataendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha shule zinakuwa salama. Wakati huohuo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na kuenea kwa kasi kwa maambukizi ya virusi vya Corona.

Nchi kadhaa za Afrika zimeanza kufungua chumi na shughuli za kawaida licha ya ongezeko la kesi za maambukizi ya corona barani humo.