Katibu Mkuu wa UN atuma salamu za rambirambi kwa serikali ya Burundi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kufuatia kuaga dunia Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa serikali ya Burundi, wananchi na familia ya kiongozi huyo.
Guterres amesisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa kuisaidia serikali na watu wa Burundi wakati huu wakipambana na janga la COVID-19, na juhudi za nchi hiyo za kuendelea kuunda taifa imara, lenye mafanikio na mustakabali wenye amani kwa raia wote. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO Burundi hadi sasa imethibitisha wagonjwa 83 wa corona na kifo kimoja.
Vyombo vya habari vimenukuu taarifa ya serikali ya Burundi ikisema kuwa, Rais Nkurunzinza aliugua na kupelekwa hospitali tarehe 7 mwezi huu wa Juni na hali yake kuimarika.
Hata hivyo mchana wa jana Jumatatu tarehe 8 hali yake ilibadilika ghafla na akapatiwa usaidizi wa mashine ya kumsaidia kupumua lakini akakata roho muda mfupi baadaye.
Tayari ya serikali ya Burundi imetangaza siku 7 za maombolezo ya kitaifa na bendera ya nchi hiyo itapepea nusu mlingoti.
Hayati Nkurunziza atakumbukwa kwa mchango wake wa kimataifa hasa wa kuwapeleka walinda amani katika nchi za Somalia na Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, kama sehemu ya vikosi vya Muungano wa Afrika pamoja na vile vya Umoja wa Mataifa.
Akituma vikosi hivyo wakati huo, Nkurunziza alisema, "kila mara Jumuiya ya Kimataifa imechangia kwa kiasi kikubwa kurejesha amani Burundi, hivyo ni wajibu kwa Burundi kulipa wema kwa kulinda amani katika maeneo mbalimbali duniani."