Jun 14, 2020 07:04 UTC
  • Raia 40, wanajeshi 20 wauawa katika hujuma nchini Nigeria

Raia zaidi ya 40 na wanajeshi wasiopungua 20 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Mashambulizi hayo yalijiri katika maeneo ya Monguno na Nganzai katika jimbo la Borno jana Jumamosi.

Walioshuhudia wanasema wanamgambo waliokuwa na silaha nzito ikiwa ni pamoja na mizinga walishambulia kituo cha wanajeshi wa serikali huko Monguno mapema asubuhi na kuua wanajeshi wasiopungua 20. Mamia ya raia wanaripotiwa kujeruhiwa katika hujuma hiyo. Aidha wanamgambo hao pia waliteketeza moto kituo cha polisi na kituo cha Umoja wa Mataifa cha kutoa misaada.

Wanagamabo hao walikuwa wamesambaza karatasi wakiwaonya wakazi wa eneo hilo wasishirikiane na maafisa wa usalama au wafanyakazi wa kimataifa wa kutoa misaada.

Hiyo jana pia wanamgambo walivamia eneo la Nganzai na kuua zaidi ya raia 40. Hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na mashambulizi hayo mawili ambayo yamekuja siku kadhaa baada ya magaidi wakufurishaji wa Boko Haram kuua raia 69 katika kijiji cha Gubio jimboni humo.

Magaidi wa Boko Haram walioanzisha uasi wao nchini Nigeria mwaka 2009 hadi sasa wameua maelfu ya watu na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kaskazini mashariki mwa Nigeria. Magaidi hao wa Kiwahhabi wameeneza uasi wao katika nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon.

Tags