Indhari kuhusu ongezeko la kasi la maambukizi ya COVID-19 barani Afrika
Mtaalamu mmoja amebainisha wasi wasi wake kuhusu ongezeko la maamubukizi ya ugonjwa wa COVID-19 barani Afrika.
Aliyekuwa mshauri wa masuala ya uchumi na jamii katika Umoja wa Afrika (AU) na pia katika Kamati ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (ECA) Costantinos Bt. Costantinos, amesema ana wasiwasi kuhusu ongezeko la kasi la maambukizi mapya ya COVID-19 barani Afrika.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kituo cha Kinga na Udhibiti wa Magonjwa barani Afrika (Africa CDC), kuanzia tarehe 2 hadi 10 mwezi huu, nchi za Afrika ziliripoti maambukizi mapya 43,182, na kuongezeka kwa asilimia 29 kuliko wiki iliyotangaulia.

Mtaalamu huyo ameonya kuwa kutokana na ongezeko la kasi la maambukizi ya COVID-19 katika wiki za karibuni, janga hilo limeathiri afya na hali ya kijamii na kiuchumi kwa watu barani Afrika.
Kwa ujumla hadi kufikia Juni 15 kulikuwa na kesi 242,969 za maambukizi ya COVID-19 huku watu 6,524 wakiwa wamefariki kutokana na ugonjwa huo na wengine 110,735 wakiwa wamepata matibabu na kupona.