DRC yaanzisha uchunguzi baada ya jaji katika kesi ya ufisadi kuuawa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61662-drc_yaanzisha_uchunguzi_baada_ya_jaji_katika_kesi_ya_ufisadi_kuuawa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imetangaza kuanzisha uchunguzi baada ya jaji Raphael Yanyi Ovungu kuuawa kwa kupigwa kichwani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 17, 2020 06:58 UTC
  • DRC yaanzisha uchunguzi baada ya jaji katika kesi ya ufisadi kuuawa

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imetangaza kuanzisha uchunguzi baada ya jaji Raphael Yanyi Ovungu kuuawa kwa kupigwa kichwani.

Yanyi ambaye alifariki dunia Mei 26 usiku, alikuwa anasimamia kesi ya Vital Kamerhe na washtakiwa wenzake. Awali polisi walikuwa wamedai kuwa jaji huyo alifariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo. Hata hivyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Sheria Célestin Tunda amesema mwili wa Jaji Yanyi ulifanyiwa uchunguzi na matokeo yake yanaonyesha kuwa alifariki dunia baada ya kupigwa kichwani.

Awali Familia ya Jaji Yanyi na wanaharakati wengine wa haki za binadamu walidai kuwa jaji huyo alipewa sumu. Waziri Tunda amesema mwili wa mwendazake haukuwa na sumu.

Rais Felix Tshisekedi wa DRC

Kifo cha ghafla cha Jaji Yanyi kilipelekea kusitishwa kesi ya ufisadi dhidi ya mpambe wa karibu wa Rais Felix Tshisekedi, Vital Kamarhe. Kesi hiyo ilianza tena Juni 3 baada ya jaji mwingine kuchukua nafasi ya Yanyi ambaye alikuwa anaongoza jopo la majaji watatu. Kamerhe anatuhumiwa kupora dola milioni 50 ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu. Kamerhe amekanusha tuhuma dhidi yake katika kesi hiyo ambayo imetajwa kuwa ni ishara ya azma ya serikali ya nchi hiyo kupambana na ufisadi.