Magaidi wa ADF waua raia 19 mashariki mwa Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61755-magaidi_wa_adf_waua_raia_19_mashariki_mwa_kongo_dr
Watu 19 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya wanamgambo wa ADF huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 22, 2020 07:40 UTC
  • Magaidi wa ADF waua raia 19 mashariki mwa Kongo DR

Watu 19 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya wanamgambo wa ADF huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Donat Kibwana, mshirikishi wa eneo la Kivu Kaskazini amesema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, viwiliwili vya raia tisa waliokuwa wametekewa nyara na wanachama wa genge hilo siku ya Ijumaa vimepatikana katika mkoa huo, mpakani na Rwanda. 

Naye afisa wa serikali katika eneo la Ituri, Bananilao Tchabi amesema raia kumi wameuawa baada ya wanamgambo wa ADF kushambulia kijiji cha Bukaka usiku wa kuamkia jana Jumapili.

Kiongozi wa asasi moja ya kiraia katika eneo hilo, Raphael Bon Benogo amesema waliouawa katika shambulizi hilo la mkoa wa Ituri ni wanaume watano, wanawake watatu na watoto wawili, na kwamba miili yao inaonesha kuwa waliuawa kwa kupigwa mapanga na wengine kwa kufyatuliwa risasi. 

Wanachama wa genge la ADF lenye asili ya Uganda

Mapema mwezi huu, watu wasiopungua 16 waliuawa katika shambulizi jingine la kutisha la wanamgambo wa CODECO huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Maelfu ya Wakongomani wameuawa katika mashambulizi ya magenge ya wanamgambo wa ADF, CODECO na magenge mengine ya waasi hususan katika maeneo ya mashariki mwa nchi, tokeo mwaka 2014.