Kituo cha kijeshi cha Uturuki nchini Somalia chashambuliwa, 2 wauawa
Kwa akali raia wawili wamepoteza maisha katika shambulizi la kigaidi lililolenga kambi ya kijeshi ya Uturuki katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Gaidi aliyekuwa amejifunga mada za milipuko alijiripua mapema jana nje ya kambi hiyo ya kijeshi ya Uturuki inayofahamika kama "Turksom" viugani mwa Mogadishu, na kuua raia wawili akiwemo mpita njia.
Msemaji wa serikali ya Somalia, Ismail Mukhtar ameliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, walinzi wa kambi hiyo walimmiminia risasi gaidi huyo ambaye alikuwa anajaribu kuingia kwa nguvu katika kambi hiyo na kumuua papo hapo. Amesema hakuna askari wa serikali ya Somalia au raia wa Uturuki aliyeuawa katika hujuma hiyo ya kigaidi.
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab kupitia radio yake ya kipropaganda ya al-Furqan limetangaza kuhusika na shambulizi hilo.
Kapteni wa Polisi, Mohamed Hussein amesema shambulizi hilo lilikusudia kuwalenga makurutu ambao walikuwa katika mazoezi yao ya asubuhi kambini hapo.
Magaidi wa al-Shabaab wanaendelea kufanya hujuma zao nchini Somalia licha ya kuweko kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini humo Amisom. Kundi hilo la kigaidi lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda linalenga kuiangusha serikali ya Somalia.