Rekodi mpya walioambukizwa COVID-19 Afrika, tahadhari yatolewa
Idadi kubwa zaidi ya walioambukizwa COVID-19 au corona barani Afrika imeripotiwa Ijumaa huku tahadahri ikitolewa kuwa ugonjwa huo unaenea kwa kasi barani humo.
Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) kimetangaza kuwa hadi Ijumaa jioni, kuliripotiwa kesi 11,219 mpya za maambukizi ya corona na vifo 216 na hivyo kuongeza idadi ya kesi hadi 348,871 na huku jumla ya waliofariki wakiwa ni 9,098.
Idadi kubwa zaidi ya maambukizi imeripotiwa katika eneo la kusini mwa Afrika ambapo Afrika Kusini inaongoza kwa maambukizi na vifo.
Hadi sasa watu wasiopungua 118,375 wameambukizwa corona Afrika Kusini huku waliofariki wakiwa ni 2,292 na waliopona wakiwa ni 59,974.

Katika taarifa siku ya Ijumaa, Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) kimesema nchi za Afrika zinapaswa kuchukua tahadhari kuhusu ongezeko la maambukizi ya corona baada ya nchi nyingi kuanza kuondoa vizingiti vilivyokuwa vimewekwa ili kuzuia kuenea ugonjwa huo.
Katika taarifa mkurugenzi wa kituo hicho cha Africa CDC John Nkengasong amesema ugonjwa wa COVID-19 ulichelewa kufika Afrika lakini maambukizi sasa yanaenea kwa kasi huku wanaofariki nao wakiongezeka.