Maelfu waandamana Darfur Sudan kulalamikia ukosefu wa usalama
Maelfu ya wakazi wa jimbo la Darfur huko Sudan wameandamana wakilalamikia kuongezeka ukosefu wa usalama na amani.
Waandamanaji hao walioandamana katika mji wa Zalingei makao makuu ya Darfur wametoa wito pia wa kukomesha vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya raia.
Wakiwa wamebeba mabango na maberamu waandamanaji hao wametaka kufutwa kazi mkuu wa mkoa huo ambaye ni mwanajeshi na nafasi yake ichukuliwe na kiongozi ambaye si mwanajeshi.
Waandamanaji hao wameapa kuwa, wataendelea na maandamano yao hadi pale serikali itakaposikiliza kilio chao na kutekeleza matakwa yao likiwemo suala la kukomeshwa machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya raia.

Mwishoni mwa maandamamano yao, waandamajai hao walikwenda na kukusanyika mbele ya jengo moja la serikali na kutoa nara za kutaka kuchukuliwa hatua dhidi ya makundi ya wabeba silaha.
Umwagaji damu unaendelea kushuhudiwa katika eneo la Darfur, licha ya serikali mpya ya Sudan kuahidi kumaliza migogoro nchini humo ukiwemo ule wa Darfur ambao umepelekea watu wasiopungua laki tatu kuuawa na wengine milioni mbili na nusu kulazimika kuwa wakimbizi.
Eneo la Darfur lilikumbwa na mgogoro kuanzia mwaka 2003 uliohusisha kundi la waasi lililodai kutengwa na utawala wa aliyekuuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir aliyeondolewwa madarakani Aprilii 11 mwaka uliopita wa 2019.