Kesi za corona zilizothibitishwa barani Afrika zapindukia 500,000
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62098-kesi_za_corona_zilizothibitishwa_barani_afrika_zapindukia_500_000
Idadi ya kesi za ugonjwa wa Covid-19 (corona) zilizothibitishwa katika nchi za Afrika kufikia leo Alkhamisi ni zaidi ya laki tano.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jul 09, 2020 11:00 UTC
  • Kesi za corona zilizothibitishwa barani Afrika zapindukia 500,000

Idadi ya kesi za ugonjwa wa Covid-19 (corona) zilizothibitishwa katika nchi za Afrika kufikia leo Alkhamisi ni zaidi ya laki tano.

Hayo ni kwa mujibu wa takwimu mpya za Shirika la Afya Duniani (WHO) ambazo zinaonyesha pia kuwa, idadi ya vifo vilivyosababishwa na maradhi hayo barani Afrika imefikia 11,930.

John Nkengasong, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) ameonya kuwa, janga la corona barani humo linashika kasi na kuna haja ya nchi za bara hilo kufanya vipimo zaidi vya ugonjwa huo wa kuambukiza.

Kituo hicho kimesema kufikia leo Alkhamisi kesi 512,499 za maambukizi ya virusi vya corona zilikuwa zimethibitishwa barani Afrika, lakini habari njema ni kwamba wagonjwa zaidi ya laki mbili na elfu 52 wa corona wamepata afueni barani humo.

 

Kipimo cha corona

Amesema kesi za corona barani humo zimeongezeka kwa asilimia 24 ndani ya wiki moja iliyopita, huku asilimia 71 ya visa vyote vya ugonjwa huo barani Afrika vikiripotiwa katika nchi za Misri, Nigeria, Afrika Kusini, Ghana, na Algeria.

Katika hatua nyingine, Kamisheni ya Umoja wa Afrika imesema ina matumaini ya kudhibitiwa janga la corona, na kwamba majaribio ya chanjo ya maradhi hayo kwa binadamu yanaendelea kufanyika hivi sasa katika nchi za Misri na Afrika Kusini.