Wagonjwa wa COVID-19 wapindukia laki saba barani Afrika
Idadi ya wagonjwa wa COVID-19 waliothibitishwa hadi kufikia jana asubuhi barani Afrika walikuwa ni laki saba na 1,573. Hayo ni kwa mujibu wa Kituo cha Kinga na Udhibiti wa Magonjwa Afrika (CDC).
Katika taarifa yake iliyotolewa jana asubuhi, kituo hicho kimesema kuwa, idadi iliyothibitishwa ya kesi za wagonjwa wa corona katika pembe mbalimbali za Afrika imeongezea kutoka wagonjwa laki sita na 83,908 iliyoripotiwa siku ya kabla yake yaani Jumamosi na imepanda hadi wagonjwa laki saba na 1573 jana Jumapili.
Kituo hicho cha kinga na udhibiti wa magonjwa barani Afrika vile vile kimetangaza kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha barani humo kwa ugonjwa huo imepanda hadi 14,937 kufikia jana asubuhi.
Ripoti ya CDC imeongeza kuwa hadi hivi sasa wagonjwa laki tatu na 69,120 wa corona wameshapata afueni barani Afrika na wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Kwa mujibu wa kituo hicho cha CDC, kasi ya maambukizo ya kirusi cha corona imeongezeka barani Afrika huku Afrika Kusini ikiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi zaidi ikifuatiwa na Misri, Nigeria, Ghana, Algeria, Morocco na Cameroon.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, eneo la kusini mwa Afrika ndilo lililoathiriwa zaidi na ugonjwa wa corona ikilinganishwa na maeneo mengine ya Afrika. Eneo la kaskazini mwa Afrika ni la pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa corona barani humo.
Eneo la magharibi mwa Afrika ni la tatu kwa kuwa na kesi nyingi za COVID-19 likifuatiwa na maeneo ya mashariki na katikati mwa bara hilo.