Rwanda: Serikali imetumia dola milioni 60 kukabiliana na Covid-19
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62332-rwanda_serikali_imetumia_dola_milioni_60_kukabiliana_na_covid_19
Wizara ya Afya ya Rwanda imesema kuwa serikali imetumia dola za Kimarekani milioni 60 ambazo ni zaidi ya faranga za nchi hiyo bilioni 54 katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 tangu kuthibitishwa kesi ya kwanza ya ugonjwa huo nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 21, 2020 10:54 UTC
  • Rwanda: Serikali imetumia dola milioni 60 kukabiliana na Covid-19

Wizara ya Afya ya Rwanda imesema kuwa serikali imetumia dola za Kimarekani milioni 60 ambazo ni zaidi ya faranga za nchi hiyo bilioni 54 katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 tangu kuthibitishwa kesi ya kwanza ya ugonjwa huo nchini humo.

Hayo yamebainishwa wazi katika mkutano na waandishi wa habari uliowakutanisha pamoja pia Mawaziri wa Afya, Serikali za Mitaa, Biashara na Viwanda na Polisi ya Taifa ya Rwanda kwa lengo la kuweka wazi namna nchi hiyo inavyokabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Waziri wa Afya wa Rwanda Dakta Daniel Ngamije amefafanua kuhusu gharama zilizotumiwa na nchi hiyo hadi sasa katika kupambana na maambukizi ya Corona. Amesema kuwa, mapambano dhidi ya maambukizi ya corona yamekuwa ya gharama kubwa kwa serikali. Ameyataja masuala mbalimbali kama upimaji wa sampuli, kujiweka mbali kwa ajili ya kuzuia kuenea maambukizi, miundomsingi na rasilimali watu kuwa ni kati ya mambo mengine yanayohitajia fedha.

Rwanda katika mapambano dhidi ya corona 

Waziri wa Afya wa Rwanda ameongeza kuwa, serikali imekadiria kutumia dola milioni 73 kukabiliana na corona katika kipindi cha miezi 6 tangu mwezi Machi mwaka huu; na kwamba hadi kufikia sasa imetumia dola milioni 60 katika uwanja huo. 

Amesema, maambukizi ya corona si tu yameiathiri serikali katika upande wa matumizi bali pia yameathiri vyanzo vya mapato. Hadi sasa Rwanda imethibitisha jumla ya kesi 1,582 za maambukizi ya corona. Watu 834 wamepata ahueni hadi sasa na watano wameaga dunia.