Maambukizi ya COVID-19 yaongezeka Afrika, yapindukia 800,000
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62442-maambukizi_ya_covid_19_yaongezeka_afrika_yapindukia_800_000
Maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 au corona barani Afrika yanaongezeka kwa kasi na hadi kufikia Jumapili waliokuwa wameabukizwa ugonjwa huo barani humo walikuwa ni 828,214.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 27, 2020 02:43 UTC
  • Maambukizi ya COVID-19 yaongezeka Afrika, yapindukia 800,000

Maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 au corona barani Afrika yanaongezeka kwa kasi na hadi kufikia Jumapili waliokuwa wameabukizwa ugonjwa huo barani humo walikuwa ni 828,214.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Barani Africa (Africa-CDC) hadi sasa waliofariki kutokana na COVID-19 barani Afrika ni 17,509 katika nchi 54 barani humo.

Eneo la kusini mwa Afrika ndilo ambalo limeathiriwa vibaya zaidi likiwa na visa 452,000 vya maambukizi ya COVID-19 likifuatiwa na eneo la kaskazini mwa Afrika lenye kesi, 147,500 huku eneo la  magharibi mwa Afrika likirekedi kesi, 118,400, Afrika Mashariki kesi 65,000, na eneo la kati mwa Afrika ni la mwisho likiwa na kesi 45,300.

Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani WHO limesema zaidi ya wahudumu wa afya elfu 10, wameambukizwa virusi vya corona barani Afrika.

Hata hivyo, idadi kamili ya watu walioambukizwa barani Afrika huenda ikawa ni ya juu zaidi tofauti na inavyoripotiwa kutokana na uhaba wa zoezi la kuwapima watu na kutokuwepo upimaji na data kamili.

Kwa ujumla takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona kote duniani imepindukia milioni 16.2 huku zaidi ya watu laki 6.48 wakiwa wameshaaga dunia hadi sasa kufuatia kuugua COVID-19.

Marekani imeendelea kuwa mhanga mkuu wa virusi vya corona ulimwenguni ambapo hadi sasa zaidi ya watu milioni nne wameambukizwa virusi hivyo nchini humo huku karibu watu laki moja na nusu wakiwa wameshafariki dunia.

Brazil ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya corona ambapo hadi sasa imesajili kesi karibu milioni 2.5 ambapo India inafuata katika orodha hiyo kwa kuwa na maambukizo karibu milioni 1.5 ya virusi vya corona.