Wafungwa wakimbia jela kaskazini mashaiki mwa DRC
Mkuu wa eneo la Watsa la kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza habari ya kutoroka jela wafungwa zaidi ya kumi nchini humo.
Christophe Ikando, mkuu wa eneo la Watsa la mkoa wa Haut-Uélé la kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa, wafungwa 12 walivunja senyenge za lango kuu la jela hiyo na kukimbia jana Jumapili. Amesema, wafungwa wengine saba bado wamo katika jela hiyo.
Duru za kuaminika zimesema kuwa, wafungwa hao wametoroka masaa 48 baada ya majaji wa mahakama ya kijeshi katika mkoa huo kufika kwa ajili ya kusikiliza kesi za wafungwa hao kwenye eneo la Watsa.
Jeshi la polisi la mkoa huo limetumwa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kubaini wafungwa hao wametoroka katika mazingira gani.
Wafungwa wa jela ya eneo hilo la Watsa wana historia ya kutoroka. Mwaka 2013 wafungwa 20 wa jela hiyo walitoroka baada ya kuvunja ukura wa jela.