Walioambukizwa corona Afrika wapindukia milioni moja
Idadi ya maambukizi ya virusi vya corona barani barani Afrika imepindukia milioni moja huku karibu ya nusu walioambukizwa wakiwa Afrika Kusini.
Shirika la Habari la AFP linasema kwa mujibu wa mahesabu yake, kesi za COVID-19 barani Afrika zimepindukia milioni moja ambapo kufikia jana Alhamisi Afrika Kusini ilikuwa na kesi 538,184 za maambukizi huku watu 9,604 wakiwa wamefariki nchini humo.
Taarifa hiyo imesema Misri ina watu 95,000 walioambukizwa na Nigeria nayo ina kesi 45,000
Kwa mujibu wa takwimu hizo, Afrika Kusini ni ya tano duniani kwa maambukizi ya corona baada ya Marekani, Brazil, India na Russia..
Pamoja na hayo bara la Afrika bado lina maabukizi ya chini ikilinganishwa na maeneo mengine ya dunia.
Hayo yanajiri wakati ambao, ripoti ya hivi karibuni imebaini kuwa asilimia 80 ya vipimo vyote vya ugojwa wa COVID-19 au corona barani Afrika vinafanyika katika nchi 10 pekee jambo ambalo linaonyesha udhaifu mkubwa katika vipimo vya corona barani humo.
Kwa mujibu wa Daktari John Nkengasong, mkuu wa Vituo vya Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa-CDC) nchi 10 za Afrika ambazo zimefanya asilimia 80 ya vipimo vya corona barani humo ni Afrika Kusini, Misri, Nigeria, Ghana, Morocco, Kenya, Ethiopia, Rwanda, Uganda na Mauritius. Amesema kila moja ya nchi hizo imefanikiwa kufanya vipimo zaidi ya 200,000 vya corona.
Kwa ujumla watu milioni 19 wameabukizwa corona duniani huku watu zaidi ya 709,000 wakiwa wamepoteza maisha hadi sasa.