Nchi 7 za Kiafrika kuanza kupima antibodi za Covid-19
Nchi saba za Kiafrika kuanzia wiki ijayo zitaanza kupima antibodi za virusi vya corona katika juhudi za kutambua kiwango cha maambukizi hayo barani Afrika.
Mkuu wa Vituo vya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) John Nkengasong amesema kuwa Liberia, Sierra Leone, Zambia, Zimbabwe, Cameroon, Nigeria na Morocco ni nchi za kwanza zilizodhamiria kufanya hivyo.
Serikali za nchi za Magharibi zinatumia vipimo vya antibodi kutambua idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona.
Hadi kufikia sasa Afrika tayari imeshafanya vipimo vya corona milioni 9.4 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 10 wiki iliyopita. Hadi jana Alhamisi bara la Afrika liliripoti kesi za maambukizi ya corona zaidi ya milioni moja na vifo vya watu 24,113.
Nkengasong amesema kuwa, nchi 25 za Kiafrika zingali zimefunga mipaka yao kikamilifu huku nchi nyingine 23 zikiendelea na zoezi la kupima watu wanaoingia katika nchi hizo kutoka nje.
Afrika Kusini inaongoza barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walioathiriwa na virusi vya corona na vilevile idadi kubwa zaidi ya watu walioaga dunia kutokana na virusi hivyo. Watu 566,109 wamepatwa na ugonjwa na COVID-19 nchini humo na 10,751 miongoni mwo wameaga dunia kuokana na virusi hivyo.