Nigeria yatishia kuwapiga marufuhu raia wa nchi zinazowazuia Wanigeria kuingia
Serikali ya Nigeria imetishia kuwapiga marufuku kuingia nchini humo raia wa nchi ambazo zinawazuia Wanigeria kuingia katika nchi hizo kutokana na janga la corona. Hayo yalisemwa jana na Waziri wa usafiri wa anga wa Nigeria, Hadi Sirika.
Hivi sasa Nigeria inajiandaa kufungua upya viwanja vyake vya ndege kwa ajili ya ndege za kimataifa. Viwanja vya ndege vya Nigeria vinatarajiwa kuanza kupokea tena wasafiri wa kimataifa tarehe 29 mwezi huu wa Agosti. Viwanja hivyo vilikuwa vimefungwa kwa ndege hizo za kimataifa tangu mwezi Machi kutokana na janga la corona.
Hata hivyo waziri wa usafiri wa anga wa Nigeria, Hadi Sirika amesema, iwapo kuna nchi zitawazuia raia wa Nigeria kuingia kwenye nchi hizo, basi serikali ya nchi yake nayo itawapiga marufuku raia wa nchi hizo kuingia Nigeria.
Juzi Alkhamisi, msemaji wa waziri huyo alikuwa amesema kuwa, sheria hiyo itazihusu zaidi ndege, si raia wa nchi hizo, hata hivyo jana Ijumaa Waziri Sirika alisema kuwa sheria hiyo itawahusu hata raia wa nchi zitakazowazuia Wanigeria kuingia katika nchi hizo.
Vile vile amesema, idadi ya wagonjwa na maambukizi ya corona nchini Nigeria ni ndogo mno ikilinganishwa na nchi za Ulaya lakini nchi hizo za Ulaya zinawanyanyapaa Waafrika wakiwemo Wanigeria kwa kuwazuia kuingia katika nchi hizo kwa madai ya kupambana na maambukizi ya COVID-19, hivyo Nigeria nayo itapiga marufuku raia wa nchi hizo kuingia nchini humo.
Hadi hivi sasa Nigeria imeripoti kesi 50,951 za wagonjwa wa COVID-19 maarufu kwa jina la corona nchini humo. Kitovu cha ugonjwa huo hatari hivi sasa ni Marekani na Ulaya.