Wafungwa 20 wauawa katika jaribio la kutoroka gerezani Madagascar
(last modified Mon, 24 Aug 2020 11:54:50 GMT )
Aug 24, 2020 11:54 UTC
  • Wafungwa 20 wauawa katika jaribio la kutoroka gerezani Madagascar

Wafungwa 20 wameuawa katika makabiliano ya risasi baina yao na askari gereza katika jaribo la kukimbia jela nchini Madagascar.

Wizara ya Sheria ya Madagascar imetangaza kuwa, ghasia hizo zilianza baada ya makumi ya wafungwa kuwapokonywa bunduki askari jela, wakiwa na lengo la kutoroka gereza la Farafangana, kusini mwa kisiwa hicho cha kusini mashariki mwa Bahari ya Hindi.

Habari zinasema kuwa, wafungwa 88 walifanikiwa kutoroka katika tukio hilo la jana Jumapili, na kwamba wengine 39 wamekamatwa na kurejeshwa jela baada ya polisi kufanya msako katika mitaa mbalimbali inayopakana na gereza hilo.

Habari zaidi zinasema kuwa, vyombo vya usalama vingali vinawasaka wafungwa wengine zaidi ya 20.

Gereza la Maison ambalo wafungwa kadhaa walitoroka miaka 3 nyuma

Mkurugenzi wa magereza katika jimbo la Atsimo Atsinanana, Nadège Patricia Razafindrakala anasisitiza kuwa, inaelekea kuwa wafungwa hao walipanga njama hiyo ya kutoroka gerezani kwa muda mrefu na wala halikuwa tukio la kushtukiza.

Visa vya wafungwa kutoroka gerezani vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara nchini Madagascar. Mwaka 2016, wafungwa 40 walifanikiwa kutoroka gereza kuu na lenye ulinzi mkali la Toliary, kusini mwa nchi.