AU yataka kupokonywa silaha raia wanaozimiliki kinyume cha sheria Afrika
Umoja wa Afrika (AU) umesisitizia udharura wa kukusanya mamilioni ya silaha zinazimilikiwa na raia kinyume cha sheria katika nchi za Afrika.
Mwito huo ulitolewa jana Jumamosi na Smail Chergui, Kamishna wa Amani na Usalama wa AU kwa mnasaba wa Mwezi wa Msamaha Afrika. Kaulimbiu ya mwaka huu 2020 ya AU ni 'Kunyamazisha (Sauti za) Bunduki, Kuunda Mazingira Rafiki Kwa Maendeleo ya Afrika.'
Kwa mujibu wa takwimu za AU za mwaka 2017, kuna silaha milioni 40 zinazobebwa na raia kinyume cha sheria barani Afrika. Idadi hiyo ni karibu asilimia 80 ya silaha zote zilizomo barani humo.
Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika amesema ni kinaya raia kumiliki kiwango kikubwa cha silaha barani Afrika ikilinganishwa na maafisa wa vikosi vya usalama. Amesema vyombo vya usalama barani humo vinamiliki silaha milioni 11 tu, ukilinganisha na milioni 40 zinazomilikiwa na raia, aghalabu yazo kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa AU, silaha ambazo zinamilikiwa na raia kwa mujibu wa sheria barani humo ni milioni 5.8, huku milioni 16 zikiwa hazijasajiliwa rasmi na vyombo vya dola. Aidha hali ya silaha zaidi ya milioni 18 barani humo haifahamiki.
Kwa mujibu wa Smail Chergui, Kamishna wa Amani na Usalama wa AU, Mwezi wa Msamaha Afrika unatoa fursa ya raia wa nchi za bara Afrika kusalimisha silaha wanazozimiliki kinyume cha sheria kwa khiari, kwa masharti kuwa wapewe kinga ya kutoshtakiwa na vilevile majina yao kutowekwa wazi.