Wanajeshi wawili wa serikali wauawa, afisa wa jeshi la Marekani ajeruhiwa Somalia
Wanajeshi wawili wa kikosi maalumu cha Somalia wameuawa na afisa mmoja wa jeshi la Marekani amejeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea leo Jumatatu nje ya kambi ya kijeshi ya kusini mwa nchi hiyo.
Mohamed Ahmed Sabriye, mkurugenzi wa mawasiliano wa jimbo la Jubbaland ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mauaji hayo yametokea baada ya mtu mmoja kujiripua na gari nje ya kambi ya kikosi hicho maalumu.
Watu wengine wawili wamejeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea kwenye kijiji cha Jana Cabdalle, yapata kilomita 60 kutoka mji wa bandari wa Kismayu wa kusini mwa Somalia. Shambulio hilo limetokea siku chache baada ya makumi ya watu kuuawa katika makabiliano makali baina ya wanamgambo wa al Shabaab na wanakijiji katikati ya Somalia.
Osman Isse Nur, msemaji wa serikali ya kieneo ya Galmudug ya katikati mwa Somalia alinukuliwa akisema juzi Jumamosi kwamba, watu 30 wakiwemo wanachama 16 wa al-Shabaab wameuawa katika mapigano hayo na kuongeza kuwa, mapigano yalianza baada ya wakazi wa kijiji cha Shabeelow kujizatiti kwa silaha na kuanza kukabiliana na wanamagambo wa al Shabaab waliowavamia kwa lengo la kuiba mifugo wao. Msemaji wa serikali ya kieneo ya Galmudug amelisema kuwa, "wanakijiji waliamua kubeba silaha na kupambana na magaidi hao kwa lengo la kuwazuia wasiwaibie mifugo yao." Kwa upande wake, Abdi Siyaad, kiongozi wa kijamii wa eneo hilo alisema wanakijiji 14 waliuawa katika mapigano hayo yaliyotokea siku ya Ijumaa na majeruhi wamelazwa katika hospitali moja mjini Galkayo.
Tangu mwaka 2007, kundi la ukufurishaji la al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani na nje ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo.