Umoja wa Mataifa wakaribisha makubaliano ya amani ya Sudan
(last modified Sun, 04 Oct 2020 11:54:40 GMT )
Oct 04, 2020 11:54 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakaribisha makubaliano ya amani ya Sudan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha kwa mikono miwili kutiwa saini makubaliano ya amani baina ya serikali ya Sudan na makundi makuu ya waasi.

Antonio Guterres amezipongeza pande zote zilizofanya juhudi za kufikiwa na kutiwa saini makubaliano hayo licha ya changamoto nyingi kama kuenea virusi vya corona.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kufikiwa makubaliano ya amani ya Juba ni sawa na kuanza kipindi kipya na kufunguliwa ukurasa mpya kwa ajili ya taifa la Sudan.

Serikali ya Sudan pamoja na makundi makuu ya waasi, jana Jumamosi yalitia saini makubaliano rasmi ya kuunda serikali ya mseto na kumaliza mgogoro wa makumi ya miaka ambao umepelekea mamilioni ya watu kuwa wakimbizi na mamia ya maelfu ya wengine kuuawa.

Mwezi Agosti mwaka huu makundi matatu makuu yalitiliana saini na Sudan makubaliano ya awali ya amani, mawili ni ya jimbo la magharibi mwa nchi hiyo la Darfur na moja ni la kusini mwa nchi hiyo. Makubaliano hayo ya awali yalitiwa saini baada ya miezi mingi ya mazungumzo yaliyofanyika katika nchi jirani ya Sudan Kusini.

Hafla ya utilianaji saini makubaliano ya amani ya Sudan

 

Kundi jingine kubwa la waasi la Sudan People's Liberation Movement-North (SPLMN) linaloongozwa na Abdelaziz al Hilu na ambalo halikushiriki kwenye hatua za awali za mazungumzo ya amani, nalo mwezi uliopita lilikubali kujiunga na mazungumzo ya amani yanayoendelea huko Sudan Kusini. 

Miongoni mwa vipengee vya makubaliano hayo ni kuingizwa jeshini wanamgambo waasi, kushirikishwa makundi ya waasi katika siasa na kupewa haki katika masuala ya uchumi na ardhi. 

Tags