Polisi visiwani Zanzibar yawaonya vikali wanasiasa 'wachochezi'
Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar nchini Tanzania amewatahadharisha wanasiasa dhidi ya kutoa matamshi ya kichochezi na uvunjifu wa amani visiwani humo, kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.
CP Mohamed Haji Hassan amesema, “baadhi ya wagombea wa vyama vya siasa wamesikika wakitamka maneno kama vile ‘wataingia barabarani’, ‘watalinda kura’, na ‘mwaka huu lazima kieleweka’. Jeshi la Polisi linaona matamshi haya ni maandalizi ya uvunjifu wa amani.”
Ameongeza kuwa, kwa sababu matamshi hayo yanakiuka Kanuni na Miongozo ya Uchaguzi Mkuu iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) pamoja na Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani (NEC), jeshi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi litachukua hatua kali kuhakikisha amani ya nchi inalindwa.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi wenye silaha za moto na mabomu ya kutoa machozi jana waliuzuia msafara wa Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tundu Lissu maeneo ya Kiluvya ukiwa unaelekea Kibaha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amesema, wamezuia msafara wa Tundu Lissu, mgombea urais kupitia CHADEMA kuendelea na ziara mkoani humo, kwa kuhofia usalama wake kwani amezuiliwa kufanya kampeni kwa siku saba.
Kamati ya Maadili ya Kitaifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) hivi karibuni ilimsimamisha Tundu Lissu kufanya kampeni kwa muda wa siku saba hadi Oktoba 9, kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu za uchaguzi.