UN: Mafuriko yameua watu 35 nchini Somalia, milioni 1.6 wameathiriwa
(last modified Thu, 29 Oct 2020 07:06:29 GMT )
Oct 29, 2020 07:06 UTC
  • UN: Mafuriko yameua watu 35 nchini Somalia, milioni 1.6 wameathiriwa

Umoja wa Mataifa umetangaza habari ya kupoteza maisha watu 35 nchini Somalia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha nchini humo.

Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, mbali na watu 35 kuaga dunia, wengine zaidi ya milioni moja na laki sita wameathiriwa na mafuriko hayo tokea Januari mwaka huu hadi sasa.

OCHA imesema watu 716,000 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mafuriko hayo, mbali na kuharibiwa maelfu ya maekari ya mashamba ya kilimo na miundombinu.

Maeneo yaliyoathirika zaidi na mafuriko hayo katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ni Puntland, Hiraan, Bakool, Galgaduud, Mudug, Nugaal na maeneo ya kusini ya Sool.

Mafuriko nchini Somalia

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu imesema kutokana na mafuriko hayo, Wasomali milioni 5.2 watahitajia misaada ya dharura ya kibinadamu kuanzia sasa hadi mwaka ujao 2021.

Aidha watu milioni 2.6 wanaishi kama wakimbizi wa ndani katika nchi hiyo ambayo mbali na mafuriko na janga la corona, inasumbuliwa pia na vita na mapigano.