Marekani sasa inaishinikiza Somalia kuanzisha uhusiano na Israel
Vyombo vya habari nchini Somalia vimeripoti kuwa, Marekani inaishinikiza nchi hiyo ianzishe uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Baadhi ya duru za kuaminika zimeripoti kuwa, serikali ya Somalia iko chini ya mashinikizo ya kisaisa na matakwa ya serikali ya Trump ili ianzishe uhusiano rasmi na Israel.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais Mohamed Farmajo wa Somalia amepinga mashinikizo hayo ya Marekani. Rais Donald Trump wa Marekani Ijumaa iliyopita alitangaza kuwa, Sudan na utawala wa Kizayuni wa Israel zimeanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia.
Hivi karibuni pia Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain zilifikia mapatano na Israel ya kuanzisha uhusiano kamili baina yao kufuatia juhudi za Marekani zenye lengo la kufanikisha mchakato wa kuanzisha uhusiano baina ya tawala za nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni. Mapatano hayo yote yamekosolewa na kupingwa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Tawala za nchi za Kiarabu zinafanya juhudi za kuanzisha uhusiano na Israel katika hali ambayo kwa miaka kadhaa sasa utawala huo ghasibu unayakalia kwa mabavu maeneo mengi ya Waraabu na Waislamu mbali na kuwakandamiza Wapalestina.