Nov 04, 2020 11:47 UTC
  • Wanachama 75 wa Boko Haram waangamizwa na jeshi la Nigeria

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuuawa makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa jeshi hilo, Benard Onyeuko amesema katika taarifa kuwa, wanachama 75 wa Boko Haram wameuawa katika kile kilichotajwa kuwa operesheni ya kusafisha mabaki ya genge hio katika eneo la kaskazini mashariki.

Amesema askari watatu wa serikali wameuawa pia katika operesheni hiyo iliyofanyika baina ya Septemba 28 na 31; na kwamba jeshi la nchi hiyo limenasa silaha na gari lililokuwa mikononi mwa kundi hilo.

Onyeuko ameongeza kuwa, vikosi hivyo vitaendeleza operesheni hiyo iliyopewa jina la 'Operation Fireball' hadi vihakikishe kuwa vimelitokomeza kikamilifu genge hilo. 

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya genge hilo la ukufirishaji kushambulia kijiji karibu na eneo la Chibok kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua watu 12 na kujeruhi wengine 7.

Baadhi ya wanachama wa Boko Haram

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kile lilichotaja kuwa kuwa huru eneo la kaskazini mwa Nigeria; na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon. 

Tangu wakati huo hadi sasa kundi hilo limeua watu zaidi ya elfu 20 na kusababisha raia wengine zaidi ya milioni mbili pia kuwa wakimbizi katika nchi hizo za magharibi mwa Afrika.

Tags