Sudan yafunga mpaka wake baada ya Ethiopia kutangaza vita na waasi
Viongozi wa serikali ya Sudan katika jimbo la Kassala wamefunga mpaka wao na Ethiopia baada ya Addis Ababa kutangaza vita na waasi wanaopigania kujitenga eneo la Tigray.
Uamuzi wa kufungwa mpaka huo umechukuliwa baada ya kuzuka mapigano baina ya jeshi la serikali na waasi wa eneo la Tigray wanaopigania kujitenga na Ethiopia.
Baada ya kupita miezi kadha ya usimamishaji vita kati yake na jeshi la serikali, kundi liitwalo Harakati ya Ukombozi wa eneo la Tigray huko Ethiopia, jana Alkhamisi lilianzisha tena vita na jeshi la nchi hiyo kwa kushambulia kituo cha eneo la kijeshi la kaskazini mwa nchi hiyo.
Serikali kuu ya Ethiopia imetangaza hali ya hatari katika eneo hilo.
Taarifa zinasema kuwa, wanajeshi 24 wa Ethiopia wamejeruhiwa katika shambulio hilo la jana. Jeshi la anga la nchi hiyo limeanzisha operesheni za kukabiliana na waasi hao wanaotaka kujitenga. Ndege za kijeshi za Ethiopia zimeshambulia vituo na maficho mbalimbali ya waasi hao katika eneo hilo la Tigray linalopakana na Eritrea.
Jana hiyo hiyo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema kuwa mashambulizi ya waasi hao yamedhibitiwa. Amesema jeshi la Ethiopia litafanya oparesheni nyingine siku chache zijazo.
Waziri Mkuu wa Ethiopia aidha alisema, jeshi la nchi yake limefanikiwa kuzima uasi wa harakati ya TPLF huko kaskazini mwa Tigray ambao ulizusha wasiwasi wa kutokea vita vya ndani. Serikali ya Addis Ababa aidha imeliweka eneo la Tigray katika hali ya hatari kwa muda wa miezi sita.