Waethiopia waanza kumiminika Sudan wakikimbia vita, wamo wanajeshi wa serikali
(last modified Tue, 10 Nov 2020 10:19:22 GMT )
Nov 10, 2020 10:19 UTC
  • Waethiopia waanza kumiminika Sudan wakikimbia vita, wamo wanajeshi wa serikali

Serikali ya Sudan imetangaza kuwa makumi ya wakimbizi kutoka Ethiopia wamevuka mpaka na kuingia kusini mashariki mwa nchi hiyo. Taarifa ya serikali ya Sudan imesema kuwa wakimbizi hao ambao wanajumuisha wanajeshi 30 wa serikali ya Ethiopia, wameingia katika eneo la Al-Luqdi mashariki mwa jimbo la al-Qadarif.

Shirika la habari la Sudan limeripoti kuwa, idadi nyingine ya wakimbizi wa Ethiopia imevuka mpaka na kuingia katika eneo la al Fashqa na kwamba maafisa wa Kamisheni ya Wakimbizi ya Sudan wanatayarisha kambi za kuwahifadhi wakimbizi hao. 

Ijumaa iliyopita viongozi wa serikali ya Sudan katika jimbo la Kassala walifunga mpaka wa nchi hiyo na Ethiopia baada ya Addis Ababa kutangaza vita dhidi ya waasi wanaopigania kujitenga eneo la Tigray.

Jeshi la Ethiopia tarehe 4 mwezi huu wa Novemba lilianza mashambulizi dhidi ya Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF)). Hujuma hiyo ilianza kwa amri ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.

Jeshi la Ethiopia

Abiy Ahmed ameongeza kuwa, serikali yake imejaribu kuepuka vita na mapigano lakini jambo hilo haliwezi kufanywa na upande mmoja. Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema kuwa hujuma ya harakati ya Ukombozi wa Tigray dhidi ya kambi hiyo ya jeshi imevuka mistari myekundu.

Abiy Ahmed pia amewataka Waethiopia kufuatilia hali ya mambo kwa utulivu na kushirikiana na jeshi la taifa.

Tags