Russia kuanzisha kambi ya jeshi nchini Sudan, itakuwa na meli za nyuklia
Serikali ya Russia imechapisha hati ya makubaliano yake ya Sudan yanayoiruhusu Moscow kujenga kambi ya kijeshi na misaada ya kilojestiki ya jeshi la majini la nchi hiyo nchini Sudan ambacho kitakuwa na askari na maafisa 300 wa kijeshi.
Kituo hicho pia kitakuwa na meli zinazotumia nishati ya nyuklia.
Waziri Mkuu wa Russia, Mikhail Mishustin amepasisha makubaliano hayo yaliyowasilishwa kwake na Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo. Sasa hati hiyo itapelekwa kwa Rais Vladimir Putin kwa ajili ya kusainiwa.
Makubaliano hayo yanasisitiza kuwa, kambi ya jeshi la Russia nchini Sudan itashughulikia masuala ya kulinda amani na usalama wa kanda hiyo ya Afrika na haitatumiwa dhidi ya nchi nyingine.
Vilevile imesisitiza kuwa, kambi hiyo inaweza kutumiwa kwa ajili ya kutoa misaada kwa meli za Russia na kwamba Sudan itakuwa na haki ya kutumia eneo la kupakulia mizigo la kituo hicho cha jeshi la majini kwa mapatano na upande husika wa Russia.
Makubaliano hayo yanasema kuwa meli zisizozidi nne zinazotumia nishati ya nyuklia zinaweza kubakia katika kituo hicho cha jeshi la majini la Russia kwa sharti la kuzingatia vigezo vya usalama na mazingira.
Novemba 17 wakati wa ziara yake mjini Moscow, rais wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir alisaini mapatano ya kupewa misaada ya Russia kwa ajili ya kusasisha jeshi la taifa la Sudan.
Moscow inafanya mikakati ya kuzidisha ushawishi wake katika bara la Afrika lenye utajiri mkubwa wa maliasili kama madini na mafuta. Russia pia ina soko kubwa la silaha katika nchi nyingi za bara la Afrika.