Sudan: Marekani ilitushinikiza tuanzishe uhusiano na Israel
Waziri wa Habari, Utamaduni na Utalii wa Sudan amefichua kuwa, Marekani iliiwekea nchi hiyo ya Kiafrika mashinikizo makubwa ya kuitaka ianzishe uhusiano na utawala haramu wa Israel.
Feisal Muhammed amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya Press TV ya Iran na kuongeza kuwa, Septemba mwaka jana 2019, nchi hiyo ilianzisha mazungumzo na Marekani juu ya kuondolewa Khartoum katika orodha ya Washington ya eti mataifa yanayounga mkono ugaidi, lakini baadaye washington ikageuza mkondo wa mazungumzo hayo.
Amesema suala lililokuwa likijadiliwa na pande mbili ni kuhusu kuzipa fidia familia za wahanga wa mashambulizi ya kigaidi yanayohusishwa na serikali ya Khartoum iliyopita, lakini baadaye kadhia ya Sudan kutakiwa ianzishe uhusiano wa kawaida na Israel ikaletwa mezani.
Waziri huyo wa Sudan amebainisha kuwa, wiki mbili kabla ya uchaguzi wa Marekani, Washigton ilishadidisha mashinikizo yake ya kuitaka Khartoum ianzishe uhusiano na Tel Aviv, na hilo lilifikiwa wiki moja kabla ya uchaguzi.
Tarehe 23 ya mwezi uliopita wa Oktoba, Wizara ya Mambo ya nje ya Sudan ilitangaza kuwa serikali ya mpito ya nchi hiyo imeafiki kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na hivyo kuifanya Sudan nchi ya tano baada ya Misri (1979), Jordan (1994), Imarati na Bahrain (2020) kufikia mapatano na Israel na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo wa Kizayuni.
Kufuatia kutangazwa uamuzi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, makundi mbalimbali ya kisiasa nchini Sudan yamepinga vikali makubaliano hayo, vikiwemo vyama washirika katika muungano unaotawala nchi hiyo.