Kiongozi wa upinzani DRC akanusha kukodi mamluki wa kigeni
Kiongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Moise Katumbi, amekanusha tuhuma zilizotolewa na serikali kuwa amekodi mamluki wa kigeni na kueleza kwamba hahofii chochote juu ya uchunguzi wa suala hilo au ripoti kwamba anaweza kutiwa nguvuni.
Katumbi ametoa matamshi hayo jana, siku moja tangu alipotangaza kuwa atagombea urais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Novemba wa kumtafuta mrithi wa Rais Joseph Kabila ambaye kikatiba anapaswa kung'atuka madarakani baada ya kukamilisha mihula miwili uongozini.
Hali ya wasiwasi imezidi kuongezeka nchini Kongo DR, kwa upande mmoja ikiwa ni kutokana na Rais Kabila kutoeleza chochote hadi sasa kuhusu hatima yake ya kisiasa. Wakosoaji wake wanasema nia yake ni kutaka kuendelea kubakia madarakani katika nchi hiyo ambayo tangu ilipopata uhuru haijawahi kushuhudia upokezanaji wa madaraka kwa njia ya amani.
Waziri wa Sheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Alexis Thambwe Mwamba amesema serikali ina ushahidi kuwa Moise Katumbi alihusika katika kusajili mamluki wa kigeni wakiwemo askari kadhaa wastaafu wa Kimarekani. Msemaji wa serikali amesema walinzi wanne wa Katumbi walitiwa nguvuni kwa sababu hawajapata kibali cha kufanya kazi nchini humo.
Hata hivyo kiongozi huyo wa upinzani amesema licha ya tuhuma na hatua hizo za serikali ataendelea na msimamo wake wa kuwania urais na kubaki kuwa mkweli kwa nchi na sheria katika harakati zake za amani.
Moise Katumbi alikuwa Gavana wa jimbo la Katanga lililoko kusini mashariki mwa Kongo DR kuanzia mwaka 2007 hadi Septemba mwaka jana alipojitoa katika chama tawala cha Rais Kabila cha PPRD akikituhumu kuwa kinapanga njama ya kuendelea kumweka kiongozi huyo madarakani.../