Maambukizi ya COVID-19 barani Afrika yaongezeka
Idadi ya walioambukizwa ugonjwa wa COVID-19 au corona barani Afrika inazidi kuongezeka.
Ripoti ya Vituo vya Kukinga na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) iinaonyesha kuwa, hadi kufikia jana Jumapili idadi ya maambukizi ya virusi vya COVID-19 au corona barani humo imefikia 2,248,269 , na watu 53,543 wamefariki dunia kutokana na virusi hivyo.
Africa-CDC imeongeza kuwa watu 1,916,227 walioambukizwa COVID-19 kote Afrika wamepona.
Afrika Kusini inaongoza kwa vifo vinavyotokana na COVID-19 barani Afrika ambapo hadi sasa watu 21, 963 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo ikifuatiwa na Misri ambayo imeripoti vifo 6,771 na Morocco vifo 6,136.
Eneo la kusini mwa Afrika limetajwa kuwa lenye kiwango cha juu zaidi cha maambukizi ya COVID-19 na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo huku eneo la kaskazini mwa Afrika likiwa la pili.
Africa-CDC ilizindua kampeni inayoitwa Wiki ya Barakoa Afrika kuanzia Novemba 23 hadi Novemba 30, ikilenga kudumisha na kuongeza uvaaji wa barakoa kama hatua ya kujilinda na virusi vya corona barani humo.
Mkurugenzi wa Africa CDC John Nkengasong amesema, hatua muhimu ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona ni kutekeleza mkakati wa afya ya jamii wa kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara na kutimiza umbali wa kijamii.
Nchi za Afrika ziko kwenye tahadhari kubwa ya kutokea wimbi la pili la mlipuko wa virusi vya corona wakati idadi ya kesi za maambukizi ya virusi hivyo barani humo imepindukia milioni mbili.