Sudan: Jeshi la Ethiopia limeua askari wetu mpakani
(last modified Thu, 17 Dec 2020 07:35:13 GMT )
Dec 17, 2020 07:35 UTC
  • Sudan: Jeshi la Ethiopia limeua askari wetu mpakani

Jeshi la Sudan limesema askari wake kadhaa wameuawa na kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa na wanajeshi wa Ethiopia wakishirikiana na wanamgambo katika mpaka wa nchi mbili hizo.

Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na jeshi la Sudan imesema kuwa, wanajeshi kadhaa wa nchi hiyo wameuawa katika shambulizi la Jumanne jioni la askari wa Ethiopia katika eneo la Abu Tyour mkoani al-Qadarif, mpakani mwa nchi mbili hizo.

Taarifa hiyo ya jeshi la Sudan haijataja idadi ya askari wake waliouawa au kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya wanajeshi wa Ethiopia.

Hata hivyo baadhi ya wanajeshi wa Sudan ambao hawakutaka kutaja majina yao wamesema idadi ya askari wa nchi hiyo waliouawa ni wanne akiwemo kamanda mwenye cheo cha Meja, mbali na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa.

Ramani ya Sudan na nchi kadhaa jirani ikiwemo Ethiopia

Sudan ilituma askari zaidi ya 6,000 katika mpaka wake na Ethiopia, baada ya kushtadi mgogoro wa eneo la Tigray. Eneo la Tigray lililoko kaskazini ya Ethiopia limeshuhudia mapigano katika wiki za karibuni kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray (TPLF).

Serikali ya Addis Ababa, ambayo inaituhumu TPLF kuwa inataka kulitenganisha eneo la Tigray na ardhi ya Ethiopia, ilitangaza hivi karibuni kuwa vikosi vya jeshi vimeudhibiti mji wa Mek’ele, ambao ni makao makuu ya eneo hilo.

Tags