Sudan imeyadhibiti maeneo yote ya mpaka wa pamoja na Ethiopia
Jeshi la Sudan kwa mara nyingine tena limeyadhibiti maeneo yote ya mpaka wa pamoja na Ethiopia; ambayo miaka 25 iliyopita yalikuwa yakishikiliwa na makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na Ethiopia.
Afisa mmoja katika mkoa wa al Qadarif huko Sudan katika mpaka wa pamoja na Ethiopia amesema kuwa, jeshi la Sudan hivi karibuni limefanikiwa kuyakomboa maeneo ya Umm Qazaz, al Asra n.k. Jeshi la Sudan katika wiki kadhaa zilizopita lilianza kusonga mbele kuelekea katika maeneo ya mpaka wa pamoja na Ethiopia ambayo kwa muda wa miaka 25 iliyopita yalikuwa yakishikiliwa na wanamgambo wa Ethiopia.
Jeshi la Sudan, limeituhumu Ethiopia na wanamgambao wanaowaunga mkono kwamba ndio walisosababisha kuuliwa na kujeruhiwa wanajeshi wa Sudan kwa kutekeleleza shambulio la kuvizia dhidi ya askari jeshi wa Sudan ambao walikuwa katika doria katika eneo la Jabal Abu Tuyur.
Kuhusiana na suala hilo, jeshi la Sudan Ijumaa iliyopita lilitoa taarifa na kusisitiza kuwa, mpaka wa Sudan na Ethiopia unafahamika na kwamba Wasudan hawatapoteza hata shibri moja ya ardhi ya nchi yao. Hii ni katika hali ambayo, kikao cha kamati ya pamoja kwa ajili ya kuainisha mipaka baina ya Sudan na Ethiopia kinafanyika leo Jumanne.
Sudan na Ethiopia zinaendelea kuhitilafiana juu ya udhibiti wa baadhi ya maeneo ya mpakani licha ya nchi hizo kuianishia mipaka yao mwaka 1902. Mivutano hiyo zaidi inatajwa kusababishwa na wakulima wa Kiethiopia ambao wamekuwa wakivuka mpaka na kuingia hadi Sudan; na kujishughulisha na kilimo. Wakulima hao wanaamii kuwa maeneo hayo ni sehemu ya ardhi ya Ethiopia.