Makumi ya wahajiri wafa maji katika pwani ya Tunisia
(last modified Fri, 25 Dec 2020 13:05:34 GMT )
Dec 25, 2020 13:05 UTC
  • Makumi ya wahajiri wafa maji katika pwani ya Tunisia

Wahajiri wasiopungua 20 wamepoteza maisha katika ajali ya boti iliyotokea jana Alkhamisi katika mji wa pwani wa Sfax nchini Tunisia.

Watu watano wamenusurika kifo katika ajali hiyo ya kuzama boti iliyokuwa imejaa kupindukia katika Bahari ya Mediterrania. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Tunisia, Mohamed Ben Zekri ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, Gadi ya Pwani ya Tunisia na wavuvi wameshirikiana kuopoa baharini miili 20 ya wahajiri walioaga dunia, na kwamba wanaendelea kusaka miili zaidi.

Inaarifiwa kuwa, boti hiyo hafifu ya plastiki iliyokuwa imebeba wahamiaji haramu baina ya 40 na 50 ilikuwa njiani kuelekea Italia kabla ya kuzama.

Mwezi Juni mwaka huu, wahamiaji wengine 54 walikufa maji katika ajali nyingine ya kuzama boti katika mji huo wa pwani ya Tunisia wa Sfax.

Miili ya wahajiri waliokufa maji ikiopolewa baharini

Wahajiri wengi haswa kutoka nchi za Afrika hupotea na kuzama baharini kila mwaka katika fukwe za Tunisia wakijaribu kuvuka kimagendo Bahari ya Mediterrania kuelekea barani Ulaya kwa tamaa ya kupata maisha mazuri, huku baadhi yao wakikimbia machafuko ya kisiasa na kijamii katika nchi zao.

Sababu nyingine ya kushuhudiwa wimbi hilo la wahajiri haramu ni uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.