Dec 27, 2020 15:28 UTC
  • Magaidi wa Boko Haram wateka nyara makumi ya wakata mbao Nigeria

Magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram wamewateka nyara wakata mbao zaidi ya 40 na kuwaua wengine watatu katika jinai yao ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa za Jumamosi, wakata mbao hao walitekwa nyara Alhamisi katika msitu wa Wulgo karibu na mji wa Gamboru katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Magaidi wa Boko Haram huwalenga wakata mbao na wakulima mara kwa mara wakiwatuhumu kuwa wanawapatia maafisa wa usalama taarifi kuhusu waliko magaidi.

Novemba mwaka 2018, magaidi wa Boko Haram waliwateka nyara zaidi ya wakata mbao na kabla ya hapo waliwaua wengine 49 katika mashambulizi mawili tafauti.

Hivi karibuni, Vyombo vya usalama vya Nigeria viliwanusuru karibu wanafunzi wavulana 350 kati ya 520 wa shule ya upili ya eneo la Kankara kaskazini magharibi mwa nchi, waliokuwa wametekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Magaidi wakufurishaji wa Boko Haram

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Halikadhalika ugaidi huo wa Boko Haram umepelekea Waislamu wa kaskazini mwa Nigeria kubakia nyuma kimaendeleo na hivyo kuathiri vibaya mustakabali wao. Serikali ya Nigeria pia inalaumiwa kwa kuzembea katika kukabiliana na magaidi hao huku kukiwa na ripoti kuwa baadhi ya majenerali jeshini na maafisa wa serikali wanaofaidika na ugaidi huo wa Boko Haram.

Tags