Jeshi la Sudan ladhibiti maeneo mapya ya waasi katika mpaka na Ethiopia
Jeshi la Sudan limedhibiti maeneo mapya yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi katika mpaka wake na Ethiopia.
Hayo yameripotiwa na televisheni ya Rusia al Yaum ambayo imeongeza kuwa, jana Jumatano, jeshi la Sudan lilitoa taarifa na kutangaza kwamba sehemu kubwa ya eneo la al Fushqa la mkoa wa al Qadarif uliko katika mpaka wa Sudan na Ethiopia, imekombolewa.
Vile vile jeshi la Sudan limetangaza kuwa sasa hivi linaendesha operesheni za kuwasafisha waasi katika eneo hilo na maeneo mengine ya mpakani.
Hayo yamekuja katika hali ambayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethipia imetoa taarifa ikililaumu jeshi la Sudan kwa kutoheshimu ujirani mwema na kuvunja sheria za kimataifa za mipakani.
Ethiopia pia imesema kuwa, jeshi lake limewekwa katika hali ya tahadhari kubwa kwenye mpaka wake na Sudan.
Wasiwasi katika mpaka wa Sudan na Ethiopia umeongezeka baada ya kutokea mapigano katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Novemba. Zaidi ya wakimbizi 50 elfu wa Ethiopia wamekimbilia katika maeneo ya mashariki mwa Sudan kukwepa mapigano hayo.
Ugomvi baina ya Sudan na Ethipia unahusiana na maeneo ya kilimo katika eneo la al Fushqa hasa baada ya wakulima kutoka Ethiopia kuyavamia maeneo hayo ya Sudan.
Hivi karibuni kuliripotiwa kutokea mapigano ya silaha baina ya wanajeshi wa Sudan na Ethiopia huku kila upande ukiushutumu upande mwingine kuwa ndio ulioanzisha mapigano hayo. Hivi karibuni pia nchi hizo mbili zilifanya mazungumzo mjini Khartoum kwa ajili ya kutatua mgogoro huo.