Khartoum yatuma zana za kijeshi katika jimbo la Darfur
Serikali ya Sudan imesema kuwa imetuma zana za kijeshi na askari jeshi wa radiamali ya haraka katika jimbo la Darfur ya Kusini ili kudumisha amani na kuwalinda raia katika eneo hilo.
Shirika rasmi la habari la Sudan, SUNA limeripoti kuwa, Hamid al Tijan Hanun Gavana wa jimbo la Darfur ya Kusini ameeleza kuwa mkoa huo ni mwenyeji wa askari zaidi kutoka kikosi cha radiamali ya haraka.

Hanun ameongeza kuwa askari jeshi hao wana kazi ya kuhakikisha kuwa sheria inatekelezwa na amani inadumishwa chini ya Mshauri wa Masuala ya Sheria katika harakati na hatua zote wanazochukua.
Eneo la kusini mwa mkoa wa Darfur ya Kusini tangu wiki mbili zilizopita hadi sasa limekumbwa na machafuko na mapigano ya kikabila kati ya makabila mawili ya al Rizigat na Fulate kusini mwa Nile. Makumi ya watu wameuliwa na kujeruhiwa katika mapigano hayo.
Katika upande mwingine, Abdulrahman Juma Kamanda wa kikosi cha radiamali ya haraka cha Sudan amezungumzia mpango huo na kueleza kuwa, idadi hiyo ya askari walioongezwa wa kikosi hicho wameshawasili katika mkoa huo ili kutekeleza majukumu yao ya kulinda amani na kuingilia haraka kwa lengo la kuepusha kujiri mapigano ya kikabila.