Umoja wa Mataifa wasisitiza kuhusu utatuzi wa kadhia ya wakimbizi Somalia
Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na wa masuala ya kibinadamu nchini Somalia amesema wakimbizi wa ndani nchini humo ni mtihani mkubwa ambao unahitaji suluhisho la muda mrefu.
Adam Abdelmoula ameyasema hayo akiwa ziarani Baidoa ambapo akiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Hataatafor amesikia mlolongo wa changamoto za wa wakimbizi hao. Miongoni mwa changamoto hizo ni malazi duni, ukosefu wa chakula na maji, upungufu wa madawa, elimu, fursa za ajira na kwa familia nyingi tatizo la ukosefu wa utulivu.
Wadau mbalimbali wakiwemo wahudumu kambini hapo, viongozi wa serikiali ya eneo hilo na wadau wa Umoja wa Mataifa aliokutana nao wote wamemuelezea changamoto hizo hizo.
Abdelmoula amewaahidi wakimbizi hao wa ndani kwamba Umoja wa Mataifa utafanya kila uwezalo kubadili maisha yao na sasa unashirikiana na serikali katika mradi wa miaka 3 unaowalenga wakimbizi wa ndani katika kusaka suluhu ya kudumu sio tu Baidoa bali pia Bosasso Puntland na Belet Weyne Hirshabelle.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaweza kushirikiana na jamii za wakimbizi wa ndani kusaka suluhu ya kudumu kwa baadhi ya changamoto sugu ambazo zinazowakabili.
Changamoto kubwa ni pamoja na vita vya miaka nenda rudi, mafuriko makubwa 19 na majira 17 ya ukame tangu mwaka 2000 ambazo zimeifanya Somalia kuwa moja ya nchi zenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani.