UN: Hali ya Tigray nchini Ethiopia inatia wasi wasi mkubwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66506-un_hali_ya_tigray_nchini_ethiopia_inatia_wasi_wasi_mkubwa
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, hali ya kibinadamu katika eneo la Tigray huko kaskazini mwa Ethiopia ni ya kutisha mno.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2021 09:54 UTC
  • UN: Hali ya Tigray nchini Ethiopia inatia wasi wasi mkubwa

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, hali ya kibinadamu katika eneo la Tigray huko kaskazini mwa Ethiopia ni ya kutisha mno.

UN imesema hayo katika ripoti yake mpya ya jana Alkhamisi na kueleza kuwa, akthari ya wakazi wa eneo hilo linaloshuhudiwa mapigano hawana chakula, maji wala mahitaji mengine ya msingi.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa, mapigano yamepelekea mamilioni ya watu katika eneo hilo washindwe kufikiwa na misaada ya kibinadamu.

Aidha miundombinu mibovu imewafanya timu za wahudumu wa asasi za kibinadamu zishindwe kuwafikishia misaada ya kibinadamu wakazi wa eneo hilo.

Eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia lilishuhudia mapigano mwishoni mwa mwaka uliopita kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF.

Wakimbizi wa Tigray wakipanga foleni kupewa chakula cha msaada

Mbali na maelfu kuuawa, wengine karibu milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Hivi karibuni, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) lilisema wakimbizi zaidi ya 20,000 wametoweka na hawajulikani waliko baada ya kambi zao mbili za Hitsats na Shimelba eneo la Tigray kuharibiwa katika mapigano baina ya waasi wa TPLF na Jeshi la Ethiopia  ambayo yalianza mwezi Novemba mwaka jana.