Rais wa Somalia: Nchi za kigeni zinavuruga mchakato wa uchaguzi nchini
Rais Muhammed Abdullahi Farmajo wa Somalia amesema uingiliaji wa madola ajinabi katika mambo ya ndani ya nchi hiyo ndiyo sababu kuu ya kugonga mwamba mazungumzo ya kujaribu kuupatia ufumbuzi mkwamo wa uchaguzi katika nchi hiyo.
Farmajo ambaye muhula wake wa kuhudumu kama rais wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika unamalizika kesho Februari 8 amelitaka Bunge la nchi hiyo liingilie kati ili nchi hiyo isitumbukie katika mgogoro wa kikatiba.
Rais Farmajo alitoa mwito huo jana Jumamosi akilihutubia Bunge la nchi hiyo, saa chache baada ya mkutano wa siku tatu baina yake na viongozi wa majimbo wa kuainisha kalenda ya pamoja ya uchaguzi nchini humo kumalizika bila natija.
Shirika la Habari la Somalia SONNA limeripoti kwamba, Rais Farmajo na viongozi hao wa majimbo hawakuweza kuafikiana juu ya mzozo wa kisiasa unaoshuhudiwa katika eneo la Gedo na mvutano baina ya wanachama wa tume ya uchaguzi wa jimbo lenye mamlaka ya ndani la Somaliland.
Farmajo hata hivyo hakutaja nchi zinazojaribu kuvuruga mchakato wa uchaguzi wa nchi hiyo ambayo pia inakabiliwa na ukosefu wa usalama kutokana na mashambulizi ya magenge ya kigaidi yakiongozwa na al-Shabaab.
Rais Farmajo na wakuu wa majimbo walikutana jijini Mogadishu mnamo Septemba 17 mwaka jana na kukubaliana juu ya mchakato wa uchaguzi, lakini tarehe ya uchaguzi wenyewe haikuweza kuamuliwa kwa sababu ya malumbano yaliyojitokeza katika mkutano huo.