Rais wa Somalia aitisha mkutano mwingine kuondoa mkwamo wa kisiasa
Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa Somalia ametoa mwito wa kufanyika kwa raundi mpya ya mazungumzo ya majadiliano tarehe 15 mwezi huu ili kusaidia kuondoa mkwamo wa mchakato wa uchaguzi.
Mazungumzo hayo yamepangwa kufanyika mjini Garowe, mji mkuu wa eneo linalojiendesha lenyewe la Puntland, baada ya mazungumzo kuhusu mchakato wa uchaguzi kati ya serikali na viongozi wa majimbo yaliyofanyika tarehe 5 Februari mjini Dhusamareb kuvunjika. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais inasema serikali kuu na serikali za majimbo zitafanya mkutano wa kilele kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa Septemba 17, 2020 kuhusu uchaguzi.
Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito kwa Serikali ya Kifederali ya Somalia kuanzisha tena mchakato wa mazungumzo ambayo yatapelekea kuwepo muafaka kuhusu uchaguzi haraka iwezekanavyo.

Wito huo umetolewa baada ya mjumbe maaulumu wa Umoja wa Mataifa Somalia James Swan kulihutubia baraza hilo na kuonya kuwa, baada ya muhula wa urais wa Farmaajo kumalizika Febrauri 8, hali ya kisiasa nchini humo haiwezi kutabirika.
Hivi karibuni Farmajo alisema uingiliaji wa madola ajinabi katika mambo ya ndani ya nchi hiyo ndiyo sababu kuu ya kugonga mwamba mazungumzo ya kujaribu kuupatia ufumbuzi mkwamo wa uchaguzi katika nchi hiyo.
Farmajo hata hivyo hakutaja nchi zinazojaribu kuvuruga mchakato wa uchaguzi wa nchi hiyo ambayo pia inakabiliwa na ukosefu wa usalama kutokana na mashambulizi ya magenge ya kigaidi yakiongozwa na al-Shabaab.