Mlipuko mwingine wautikisa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu; watu kadhaa wauawa
Kwa akali watu watatu wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko mkubwa katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.
Duru za usalama za Somalia zinaserma kuwa, mlipuko huo umetokea mapema leo jirani na ikulu ya Rais mjini Mogadishu.
Taarifa ya wanausalama kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa, gari lililokuwa na mada za milipuko lilipita kwa kasi katika kituo cha upekuzi na kuelekea ilipo ikulu ya rais ambapo polisi ililifyatulia risasi.
Dereva wa gari lililotekeleza shambulio hilo la kigaidi ameangamia katika mlipuko huo wa kujitolea muhanga. Kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda hadi sasa limeshakiri kuhusika na matukio mengi ya utegaji mabomu na mashambulio ya kigaidi ndani ya Somalia na katika nchi jirani. Hadi sasa hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulio hilo, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba limefanywa na kundi la kigaidi la Ash-Shabaab.
Somaalia
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la Ash-Shabaab limekuwa likiendesha harakati za mtutu wa bunduki kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya Somalia.
Mwaka 2011, jeshi la Somalia likisaidiwa na vikosi vya Umoja wa Afrika vinavyojulikana kama AMISOM lilifanikiwa kuwatimua magaidi wa Ash-Shabaab katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
Somalia inaendelea kuandamwa na machafuko na mauaji huku muda wa Rais Mohamed Abdullahi Farmajo ukiwa umemalizika tangu tarehe nane ya mwezi huu wa Februari.
Hivi majuzi Rais Farmajo alitoa mwito wa kufanyika kwa raundi mpya ya mazungumzo ya majadiliano tarehe 15 mwezi huu ili kusaidia kuondoa mkwamo wa mchakato wa uchaguzi wa nchi hiyo.