Mamia ya maelfu washiriki katika mazishi ya kihistoria ya Maalim Seif Sharif Hamad, Zanzibar
(last modified Thu, 18 Feb 2021 17:58:25 GMT )
Feb 18, 2021 17:58 UTC
  • Mamia ya maelfu washiriki katika mazishi ya kihistoria ya Maalim Seif Sharif Hamad, Zanzibar

Mamia ya maelfu ya Watanzania hasa wa Visiwa vya Zanzibar leo wameshiriki kwenye maziko ya kihistoria ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad yaliyofanyika katika kijiji alikozaliwa cha Nyali huko Mtambwe kisiwani Pemba.

Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alikuwa pia Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo alifariki dunia jana saa za asubuhi katika hospitali ya taifa ya Muhimbili mjini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Shughuli za mazishi ya Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar zilianza mapema leo asubuhi katika msikiti wa Maamur mjini Dar es Salaam ambako mwili wa marehemu ulioshwa na kukafiniwa kabla ya kusaliwa katika miskiti huo katika Sala ya maiti iliyoongozwa na Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali na kuhudhuriwa pia na viongozi kadhaa wa serikali wakiwemo marais wastaafu wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Mrisho Kikwete.

Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad

Baada ya sala hiyo, mwili wa marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ulisafirishwa kuelekea kisiwani Unguja ambako alisaliwa katika viwanja vya Mnazimmoja katika Sala iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wakiongozwa na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi pamoja na viongozi wengine wakuu wa serikali.

Kutoka viwanja vya Mnazimmoja, mwili wa marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ulisafirishwa kuelekea kisiwani Pemba ambako huko pia alisaliwa Sala ya maiti iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa kisiwa hicho katika viwanja vya Gombani, mjini Chake Chake wakiongozwa na Rais Mwinyi pamoja na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe.

Marehemu Maalim Seif (kulia) na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

Msafara uliobeba mwili wa mwanasiasa huyo mashuhuri na mkongwe katika visiwa vya Zanzibar na Tanzania ulielekea katika kijiji cha Nyali huko Mtambwe, katika wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba ambapo baada ya kusaliwa katika msikiti wa kijijini hapo Maalim Seif alikamilisha safari ya maisha yake duniani kwa kuzikwa kijijini kwao hapo alipozaliwa.

Marehemu Maalim Seif Sharif, ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 78 anatajwa kama mmoja wa wanasiasa wachache barani Afrika waliotukuka kisiasa kwa kutoguswa na kashfa za ufisadi katika maisha yake ya kisiasa, mbali na kutoacha rekodi yoyote ya kujilimbikizia utajiri yeye mwenyewe au kwa kutumia jamaa na watu wake wa karibu. Alikuwa kiongozi aliyependwa na Wazanzibari wengi licha ya kumaliza maisha yake ya kisiasa kwa kutotimiza ndoto aliyokuwa nayo ya kuiongoza Zanzibar kama rais wa nchi.

Maziko ya Maalim Seif Sharif Hamad

Katika Zanzibar ambayo imeshuhudia taharuki na machafuko ya kisiasa katika takriban kila uchaguzi tangu ulipoanzishwa tena mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania mwaka 1992, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad atakumbukwa na wengi kwa juhudi zake za kuchangia kupatikana maridhiano ya kisiasa katika visiwa hivyo ambavyo ni moja ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya uchaguzi wa Oktoba 2020, ambao ulishuhudia machafuko makubwa yaliyosababisha pia watu kadhaa kuuawa na kujeruhiwa, Maalim Seif Sharif Hamad alionyesha tena ukomavu na uvumilivu wa kisiasa kwa kufanikisha kupatikana ridhaa ya chama chake kujiunga katika serikali ya umoja wa kitaifa ya Zanzibar iliyoasisiwa kikatiba kwa juhudi za mwanasiasa huyo na aliyekuwa Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume na kuanza kufanya kazi rasmi baada ya uchaguzi wa 2010.

Rais Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akipeana mkono na Maalim Seif Sharif baada ya kumwapisha kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

Wakati akitoa taarifa rasmi ya serikali juu ya kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad hapo jana, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi, alimtaja marehemu kwamba alikuwa kiongozi mzalendo na shupavu.

Kufuatia kifo cha Maalim Seif Sharif, Rais wa Zanzibar ametangaza siku saba za maombolezo visiwani humo na Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa Tanzania nzima.../