Magaidi 52 wa Ash-Shabaab waangamizwa kusini mwa Somalia
Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Somalia ametangaza kuwa, wanamgambo 52 wa kundi la kigaidi la Ash-Shabaab wakiwemo vinara wawili wa kundi hilo wameuawa kusini mwa nchi hiyo.
Brigedia Jenerali Odowaa Yusuf Rageh ameiambia redio la jeshi la taifa kwamba, vikosi vya jeshi hilo vimefanikiwa kuwaangamiza wanamgambo 52 wa kundi la kigaidi la Ash-Shabaab katika operesheni ya shambulio iliyofanywa dhidi ya ngome ya kundi hilo katika eneo la Shabelle ya Chini kusini mwa nchi hiyo.
Jenerali Rageh ameongeza kuwa, katika operesheni hiyo, vikosi vya jeshi la serikali vimeteketeza pia maficho madhaa ya magaidi wa Ash-Shabaab.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi na ukufurishaji la Ash-Shabaab limekuwa likiendesha kampeni ya mtutu wa bunduki kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya Somalia.
Mnamo mwaka 2011, kundi hilo la kigaidi lilitimuliwa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kwa operesheni za pamoja za mashambulio zilizotekelezwa na jeshi la serikali likisaidiana na vikosi vya kijeshi vya Umoja wa Afrika AMISOM; lakini hadi sasa lingali linaendelea kudhibiti sehemu nyingi za maeneo ya vijijini ya nchi hiyo.../